Saturday, June 25, 2011

Nisha: Wasanii tusiridhike mapema

MSANII anayekuja juu kwenye fani ya filamu nchini, Salma Jabu 'Nisha' amewataka wasanii wenzake kutoridhika na mafanikio ya kutamba nyumbani na badala yake kujibidiisha kujitangaza katika anga la kimataifa.
Nisha aliyeng'ara kwenye filamu kama 'Family Disaster', 'Better Day', 'Kimya' na nyinginezo, alisema kulewa sifa na mafanikio ya nyumbani kwa wasanii wengi nchini kunachangia wengi wao wasitambe kimataifa, kitu kinachopaswa wabadilike sasa.
"Wasanii nchini wanapaswa kubadilika na kujitangaza kimataifa, tusiridhike na mafanikio ya nyumbani kwani ndio yanatufanya tusipige hatua kubwa kimaendeleo kama wenzetu wa nje,' alisema Nisha, aliyejitumbukiza kwenye fani hiyo miaka mitatu iliyopita.
Nisha ambaye yupo mbioni kuibuka na filamu iitwayo 'Simu Sikioni' ya msanii nguli, Deo Shija, alisema hata yeye mwenyewe pamoja na nyota ya neema kuanza kumulikia kwa sasa nchini, hataridhika hadi atakaposimama kimataifa akichuana na wakali wa dunia katika fani hiyo.
"Ndoto zangu ni kutamba kimataifa kwa kuwa sitaridhika na mafanikio ya nyumbani, jambo ambalo kila msanii wa ukweli anatakiwa awe hivyo," alisema Nisha.
Mzanzibar huyo, alisema anaamini kama kila msanii atakuwa na kiu ya kutamba kimataifa  ni wazi Tanzania itajitangaza na kutoa fursa ya Watanzania kutambulika kama ilivyo kwa Wanigeria, Wamarekani na wasanii wengine wanaotamba ulimwenguni.

No comments:

Post a Comment