WAZIRI wa Kazi na Ajira, Mhe. Gaudencia Kabaka amewataka waajiri wa Mashirika binafsi nchini kuwapa wafanyakazi wao mafunzo ya kuwaongezea ujuzi badala ya kuwaacha waendelee kubaki walivyo kwa kuhofia gharama za mafunzo hayo.
Waziri huyo aliyasema hayo alipokuwa mgeni rasmi katika mkutano wa Chama cha Waajiri Nchini, ATE, uliofanyika jijini Dar es Salaam na kudai waajiri wengi kwa sasa wanaajiri watu kutoka nje kwa kuhofia kuwaendeleza waliopo ambao huwa na kiwango kidogo cha elimu kukwepa gharama za kuwaelimisha.
"Inaonekana waajiri hasa wa sekta binafsi hawatoi mafunzo kwa wafanyakazi wao ila wapo tayari kuchukua wafanyakazi waliokwisha pata mafunzo kutoka nje ya mashirika yao kwa kuhofia gharama," alisema.
Alisema kuwa, mafunzo kwa waajiriwa husaidia kuwaongezea ujuzi katika utendaji wao na hivyo kupanua wigo wa kufikia maendeleo yanayootwa na mashirika hayo kuliko kukwepa jukumu hilo kwa kukimbilia waajiriwa wa kigeni.
Waziri alisema kampuni zote duniani huwa na malengo yake kibishara, lakini huweza yasifikiwe kama kampuni au mashirika hayo hayawaongezei ujuzi watendaji wake, na kusisitiza umuhimu wa waajiri kuzingatia hilo.
Aidha alisema serikali ina lengo kwamba ifikapo mwaka 2025 iwe imeboresha elimu na mafunzo katika jamii pamoja na ujenzi wa uchumi imara na wenye ushindani.
Naye Mwenyekiti wa Chama hicho, Cornelius Kariwa aliitaka serikali kupunguza gharama za uendeshaji wa biashara nchini ili kuweza kumudu ushindani wa kibiashara kwa sasa na kuvutia uwekezaji nchini
Alisema kwa sasa mfanyabiashara analipa kiasi cha asilimia sita ya mshahara wake, hali inayosababisha kukua kwa gharama ya juu ya biashara yake ukilinganisha na nchi nyingine.
Alisema, kauli mbiu ya chama hicho kwa mwaka 2011 ni "Kuwekeza Katika Rasilimali Watu ni Chachu ya Kuongeza Uzalishaji Katika Nchi Yetu'.
No comments:
Post a Comment